Wednesday, December 7, 2011

MAKAMU WA RAIS DK GHARIB BILAL AHUDHURIA MKUTANO WA 17 WA MABADILIKO YA TABIANCHI DURBAN-AFRIKA YA KUSINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza wakati wa mkutano wa majadiliano wa Viongozi wakuu 194 wa nchi wanachama wa Itifaki wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya Tabianchi, juu ya kupunguza uzalishaji wa gesijoto Duniani kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa 17 wa umoja huo uliofanyika jana Desemba 6 mjini Durban, Afrika ya Kusini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano wa Viongozi wakuu wa Nchi wanachama 194 wa Itifaki wa umoja wa mataifa wa mabadiliko ya Tabianchi, juu ya kupunguza uzalishaji wa gesijoto Duniani kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa 17 wa umoja wa mataifa wa mabadiliko ya Tabianchi Duniani uliofanyika jana Desemba 6, mjini Daban. Picha na Amour Nassor-Ofisi ya Makamu wa Rais
---
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AHUDHURIA MKUTANO WA MAZINGIRA DURBAN (COP 17) DESEMBA 07, 2011
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal anahudhuria mkutano wa dunia wa Mazingira unaofanyika nchini Afrika Kusini katika jiji la Durban ukiwa na agenda nzito kuhusu mchango wa matafia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Tangu maandalizi ya mkutano huu kuanza mwanzoni mwa mwaka, kumekuwa na makundi mbalimbali yanayozungumzia namna ya kuiweka dunia katika hali shwari sambamba na kuhakikisha uharibifu wa mazingira hauendelei kwa kuwa madhara yake yanaonekana katika kila kona ya dunia, japokuwa ukweli unabakia kuwa mchango wa kila taifa katika kuharibu hali ya mazingira ya dunia si sawa na wachangiaji wakubwa wa uharibifu wanabaki kuwa mataifa makubwa yaliyoendelea kiuchumi.
Makamu wa Rais Dkt. Bilal aliungana na viongozi wa nchi mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma katika meza ya mjadala kuhusu dunia tunayoitaka mjadala ambao pia ulimshirikisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Jean Ping. Katika mjadala huu mataifa yaliyoshiriki yalikubaliana kwa kauli moja kuwa, COP 17 itoke na maamuzi ambayo yatasawiri safari ya maamuzi yaliyosainiwa katika Protokali ya Kyoto na sio kumaliza maamuzi ya protokali hiyo
“Nikiwatazama wote mliopo hapa naona suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi, naona kuna kila sababu ya mkutano huu kutoa majibu ya siku zijazo na hivyo kuondoa hofu inayokabili dunia kwa sasa na siku zijazo,’ alisema Rais Zuma wakati akifungua kikao cha COP 19, CMP 7 ambacho kinahusisha utoaji wa kauli za kila nchi mshiriki wa mkutano huo, zilizoanza kutolewa jana.
Katika mkutano huu Tanzania licha ya kuwa na ushiriki wa Makamu wa Rais ambaye pia anasimamia Mazingira na Muungano, pia yupo Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt. Terezya Huvisa ambaye amekuwepo hapa kufatilia vikao katika ngazi ya mawaziri akiwa na wataalamu wake sambamba na Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Julius Ningu. Pia yupo Waziri wa SMZ katika Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Fatma Fereji na wataalamu wengine katika eneo hili la mazingira pamoja na asasi za kiraia kutoka Tanzania.
Mkutano wa COP 17, unakabiliana na ugumu kufuatia nchi tajiri hasa Marekani, Japan na Umoja wa Ulaya kutoonyesha kukubaliana kwa haraka kuhusu kusaini Protokali ya Kyoto. Mataifa haya ndiyo yaliyonufaika na yanayonufaika na uchangiaji wa gesi zinazoharibu hali ya hewa duniani, jambo linalofanya mataifa maskini sasa kukabiliana na changamoto kubwa kama ile ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha ukame na mafuriko na kuhatarisha maisha ya wananchi wengi duniani. Nchi za Afrika zinahitaji mataifa makubwa kulipa kutokana na madhira waliyosababisha na kilio hiki kinaonekana bado kinachukua muda mrefu kupatiwa jibu, kwa kuwa nchi tajiri sasa hivi nazo zinajitetea kutokana na kukabiliana na mporomoko wa uchumi katika nchi zao.
Mkutano huu ni wa kwanza kufanyika Afrika na unaonyesha namna bara hili linavyokua kwa kasi huku likiwa na watu walio tayari kutafuta mabadiliko licha ya kuwa nchi nyingi katika bara hili bado zinakabiliwa na umaskini unatokana na sababu nyingi na kubwa zikiwa hizi za kusababishiwa umaskini na mataifa nje, ambayo yamegeuza nchi za Afrika kuwa sehemu za kutupia taka ambazo huangamiza mazingira.
Imetolewa na:
Idara ya Habari Ofisi ya Makamu wa Rais
Durban, Desemba 07, 2011

No comments: