Friday, December 23, 2011

POLISI MKOA MJINI MAGHARIBI ZANZIBAR WATAJWA KULETA MAFANIKIO KATIKA HUDUMIA YA MWANAMKE NA MTOTO

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zainzibar imesema mpango wa kuanzishwa kwa dawati linaloshughulikia kesi za kijinsia kwenye vituo vya Polisi hapa nchini kumeongeza uhuru zaidi wa kujieleza kwa watu wanaodhalilishwa na kufika Polisi kuomba huduma za kisheria.

Mkurugenzi wa Idara ya Ustawa wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar Bi. Halima Khamis, ameyasema hayo wakati alipotembelea Ofisi za Dawati la Polisi mkoa wa Mjini Mgharibi Zanzibar ambapo aliwaongoza wageni kutoka mashirika ya mbalimbali ya Kimataifa kuja kuona mafanikio yaliyopatikana katika ofisi za Dawati hilo.

Mkurugenzi huyo amesema tangu kuanzishwa kwa Dawati hilo katika mkoa wa Mjini Magharibi, Idara ya Ustawi wa Jamii Visiwani Zanzibar imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa katika kupata ufumbuzi wa kesi za ukatili wa kijinsia.

Bi Halima amesema uwezo wa kiutendaji unaonyeshwa na Askari walipo kwenye ofisi za Dawati la Wanawake na Watoto mkoa wa Mjini Magharibi, umesaidia kuiwezesha jamii kupata huduma bora na kwa wakati jambo ambalo amesema limechangia kuamsha ari za mapambono dhidi ya matendo ya kikatili kwa wanaweke na watoto Visiwani hapa.

Amesema Ofisi hizo zimekuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali wa Kimataifa wanaotembelea Visiwani Zanzibar wakitaka kutembelea pia katika ofisi hizo kwa nia ya kujifunza zaidi.

Wakati wa Mkutano wao, Mratibu Msaidizi wa Dawati hilo Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar Inspekta Fakih Yusufu Mohammed, aliwaambia wageni hao kuwa, pamoja na changamoto zilizopo, lakini Dawati hilo limepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwezi Aprili mwaka jana (2010).

Inspekta Fakih amesema kuwa umuhimu wa Dawati hilo umefahamika baada ya watu mbalimbali kupatiwa huduma na elimu juu ya mapambano dhidi ya vitendo vya kikatili wa kijinsia.

Amesema hivi sasa idadi ya watu wanaofuata huduma za kisheria katika ofisi za Dawati imeongezeka kutoka watu 11 wa mwaka jana lilipoanzishwa mwaka jana hadi kufikia watu 55 mwaka huu wa 2011.

Ameyataja mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kutoa mwamko kwa wananchi wanaopatwa na matatizo ya unyanyasaji kijinsia kujitokeza kutoa taarifa Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe .

Amesema siku za nyuma matatizo kama hayo yalikuwa yakimalizwa katika ngazi ya familia tofauti na sasa ambapo mtazamo huo umebadilika kutokana na elimu inayotolewa juu ya madhara yatokanayo na matendo kama hayo siku za usoni.

Awali akizungumza na ujumbe huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa bado Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajitokeze kutoa kutoa taarofa Polisi na kwenda Mahakamani kutoa ushahidi pale wanaposhuhudia vitendo vya udhalilishwaji wa kijinsia kwa mwanamke na watoto.

Kamanda Aziz amesema kuwa matendo mengi ya kikatili yanafanywa na watu wa familia moja na hivyo kuwafanya watendewa wa makosa hayo na mashahidi kutochukua hatu kwa kuhofia kuwa wakijulikana wataweza kukamatwa na kufikishwa mahakamani na hata kufungwa jela.

Katika ziara hiyo, Bi. Halima alifuatana na wageni kutoka Shirika la Midaasa la Marekani USAID, Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Afya za Familia FHI na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.

No comments: