Monday, December 12, 2011

Polisi wamkamata tena Mbowe, ahaojiwa na kuachiwa



Mbunge wa Hai (Chadema), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, jana alishikiliwa na jeshi la polisi kwa takribani robo saa kwa mahojiano baada ya kupiga fataki katika maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa kwake bila kuwa na kibali cha kupiga fataki hizo.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa nne usiku katika ofisi za Hai Kilimanjaro Development Initiative ambapo alifanya tafrija ya kujipongeza kwa kutimiza miaka hiyo ya kuzaliwa kwake na ndipo askari walipofika na kumchukua kwa ajili ya mahojiano.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi, ni kwamba mbunge huyo alifanya hivyo kinyume na taratibu na pasipokuwa na kibali kutoka kwa jeshi hilo.

Taarifa hizo zilieleza kwamba baada ya kuhojiwa kwa muda, Polisi walimwachia.
Kwa upande wao, wananchi waliozungumza na NIPASHE, walilaani kitendo cha polisi kumkamata mbunge huyo na kusema kuwa ni kumnyanyasa kisisasa na kumyima uhuru wa kusheherekea siku yake ya kuzaliwa.
John Mbowe na Mama Salama, waliliambia gazeti hili kuwa kitendo hicho ni cha kumdhalilisha na kulidhalilisha jeshi hilo kutokana na ukweli kuwa kupiga fataki tena katika maeneo ya wazi si kosa na kuongeza kuwa wapo watu wengine wamekuwa wakipiga fataki na hawakamatwi.
Kwa upande wake, Mbowe hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kutokana na kuwa na shughuli nyingi ambapo alikuwa akielekea kwenye
harambee ya kuchangia upanuzi wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Nshara.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wilaya ya Hai, Revocatus Malin ili azungumzie tukio hilo, ziligonga mwamba kutokana na kutokuwepo ofisini wakati Kamanda wa polisi mkoani hapa, Absalom Mwakyoma hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: