Thursday, December 22, 2011

Serikali Ya Mapinduzi Zanzibar Yatoa Salam Za Rambirambi Kwa Wakazi Wa Dar


Na Zahira Bilal Maelezo Zanzibar 22/12/2011

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa Mkono wa Pole kwa wale wote waliopatwa na ajali na kupoteza jamaa zao kutokana na Maafa makubwa ya mafuriko yaliyosababishwa na Mvua zinazoendelea kunyesha katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema Zanzibar imeguswa na msiba huo na kuwaombea majeruhi wa janga hilo wapone haraka na wale waliopoteza ndugu na jamaa kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki kigumu.

Aidha taarifa hiyo inasema kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar Mvua kubwa zitaendelea kunyesha katika maeneo ya Dar es Salaam na maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba kwa muda wa siku tatu zijazo.

Kutokana na hali hiyo wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari kwa kusafisha mitaro iliyoziba na kuondoka katika maeneo yanayotuama maji ili kuepuka na maafa ambayo yanaweza kujitokeza

Pia taarifa hiyo imewataka wananchi kufuata kanuni za afya ikiwemo kuchemsha maji ya kunywa na kuweka usafi katika maeneo yao ili kujihadhari na maradhi ya miripuko.

Kwa upande wa watumiaji wa Bahari taarifa hiyo imewataka wananchi kusikiliza utabiri wa hali ya hewa kabla ya kufanya shuguli zao za baharini ikiwa ni pamoja na uvuvi na usafiri.

Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 13 na kuharibu miundo mbinu pamoja na makaazi ya watu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara hasa katika Jiji la Dar es Salaam.

MWISHO
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments: