Monday, December 26, 2011

Vibaka wapora magodoro ya waathirika wa mafuriko Dar

Zoezi la ugawaji misaada katika vituo vya waathirika wa mafuriko ya mvua kubwa zilizonyesha jijini Dar es Salaam mapema wiki iliyopita, limeingia dosari katika kituo cha Hananasif baada ya kundi la vijana wasiofahamika kuvamia kituo hicho na kupora magodoro 50.
NIPASHE ilifika katika kituo hicho na kukuta malalamiko kadhaa kutoka kwa waathirika hao.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alithibisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kundi la watu wasiofahamika lilivamia kituo cha Hananasif na kupora magodoro 50 na kuongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kuwabaini waliofanya uhalifu huo.

Awali, Diwani wa Kata ya Hananasif, Abbas Tarimba, alithibitisha kutokea wizi huo na kueleza kuwa usiku wa kumkia jana, watu wasiofahamika walianzisha fujo na ndipo walipopata mwanya wa kuiba magodoro hayo.
Alisema fujo hizo zilianza wakati wa zoezi la ugawaji wa magodoro kwa waathirika ambapo katika hali ya kushangaza, idadi kubwa ya watu iliongezeka ghafla kwenye kituo hicho.
Kadhalika, alisema kituo hicho kinakabiliwa na ongezeko kubwa la waathirika kila kukicha kutokana na kugawa chakula kila siku hali inayosababisha walengwa kukosa huduma.
Mbali ya Hananasif, vituo vingine pia vimekumbwa na adha ya wananchi ambao hawakupatwa na janga hilo kufika kwenye kambi zinazowahudumia waathirika nyakati za jioni ili wanufaike na misaada inayotolewa vikiwemo vyakula.
Kituo kingine kinachokabiliwa na changamoto hiyo ni cha Shule ya Uhuru Mchanganyiko, ambako wananchi wasio waathirika wamekuwa wakienda kituoni hapo kwa nia ya kugawiwa vyakula vya msaada.
Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Utawala na Utumishi, Ellyn Mcha, alisema: “Nyakati za chakula idadi ya watu hapa ni kubwa ikilinganishwa na wakati ambao si wa kula.”
Hata hivyo, katika kituo hicho zoezi la ugawaji wa misaada linaendelea vizuri na hakuna na malalamiko yoyote kutoka kwa waathirika.
Wakati huo huo, hali si shwari katika kambi ya Mchikichini baada ya waathirika kuendelea kugoma kuondoka katika kambi hiyo kufuatia agizo la Serikali kutaka kuwahamishia kituo cha Shule ya Uhuru na katika Sekondari Benjamin Mkapa.
NIPASHE ilifika katika eneo hilo na kukuta umati mkubwa wa waathirika ukiwepo hapo ambapo ilizungumza na mmoja wao, Mnyusi Mohamed, aliyeeleza kuwa katu hawawezi kuondoka eneo hilo kwa kuwa wanahofia mali zao kuibiwa.
Alisema eneo hilo ni mwafaka kwao kwa sababu ni karibu na nyumba zao ambapo licha ya kuwa kambini, wanazilinda.
Magongwa Emmanuel, alilalamikia zoezi la ugawaji wa misaada akieleza kuwa sio mzuri kwa sababu idadi ya waliopata ni ndogo kuliko ambao hawajapata.
Kwa upande wake, Mganga wa Kituo cha Afya cha dharura kilichopo katika kituo cha Uhuru, Dk. Julius Keto, alisema wamepokea wagonjwa wenye matatizo madogo madogo kama vile kujikata na chupa, presha lakini hakuna magonjwa ya mlipuko.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadick, amewaasa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wasikiapo harufu mbaya ikitoka mabondeni.
Alitoa ufafanuzi huo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi walioeleza kuwa kumekuwa na harufu mbaya kutoka maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hali inayoashiria kwamba kuna miili ya watu imenasa kwenye tope.
“Hizo taarifa za miili kunasa sio za kweli Jeshi la Polisi limefuatilia na limekuta wanyama kama mbuzi na mbwa ndio wamekufa lakini wananchi wasisite kutoa taarifa wanapohisi harufu mbaya,” alisema Sadick.
Aliongeza kuwa hadi jana hakukuwa na ongezeko lolote la vifo wala majeruhi.
Hadi sasa mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 38.
CHANZO: NIPASHE

No comments: