Tuesday, January 31, 2012

201 WAAGA DUNIA KUTOKANA NA MGOMO WA MADAKTARI




Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa

MGOMO
wa madaktari unaoendelea nchini tangu Jumatatu ya wiki iliyopita,
inasemekana umesababisha vifo vya wagonjwa wanaokadiriwa kufikia 201.

Uchunguzi
uliofanywa na timu ya Uwazi tangu mgomo huo ulipoanza, umegundua
kwamba kiasi hicho cha wagonjwa waliokufa ni katika mikoa inayokabiliwa
na tatizo hilo la madaktari kugoma.
Waandishi wetu Dar es Salaam,
walitembelea wodi kadhaa na vyumba vya kuhifadhia maiti vya Hospitali
za Temeke, Amana, Mwananyamala na Muhimbili kujionea athari za mgomo
huo, huku wa mikoani nao walifanya hivyo.

MUHIMBILI
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
umebaini kuwa wagonjwa wengi wameathiriwa na mgomo huo hali iliyowafanya
wajazane wodini bila kupata tiba.
Aidha, timu yetu ilishuhudia
wagonjwa wengi wakiwa wamelala chini kwenye korido huku wakiugulia
maumivu kwa kukosa huduma ya madaktari.

Akizungumza na gazeti hili
wiki iliyopita mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Samson
Maandizi, aliyelazwa Wodi ya Sewahaji alisema tangu alipofika
hospitalini hapo kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali ya gari,
hajawahi kupata matibabu.
Kufuatia hali tete ya kimatibabu
iliyosababishwa na mgomo huo, baadhi ya wananchi wamelazimika
kuwahamisha wagonjwa wao na kuwapeleka katika hospitali binafsi.

Hata
hivyo, mwananchi mwingine, Hamisi Juma alipohojiwa na gazeti hili
hospitalini hapo alisema: “Kutokana na kutokuwa na fedha nimeamua
kumhamisha mama yangu na kumpeleka kwa mganga wa kienyeji Mbagala.” Kwa
upande wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo, mhudumu ambaye
hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kwamba tangu mgomo huo
uanze idadi ya waliokufa mpaka juzi (Jumapili) wanaweza kufikia 57.

MWANANYAMALA
Kwa
upande wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya
Mwananyamala, mmoja wa wahudumu alisema kwamba idadi ya waliokufa kwa
kipindi hicho wanaweza kufikia 20.

AMANA
Katika Hospitali ya Amana mhudumu wa chumba cha maiti amesema tangu mgomo huo ulipoanza, watu waliofariki wanaweza kufikia 15.

TEMEKE
Nayo
Hospitali ya Temeke hali ni tete kwani inadaiwa nako wagonjwa 19
wamefariki dunia kipindi cha mgomo, kwa mujibu wa mtumishi mmoja wa
hospitali hiyo.

BUGANDO MWANZA
Katika Hospitali ya Bugando
Mwanza, mmoja wa wahudumu wa chumba cha maiti alimwambia mwandishi wetu
mjini humo kwamba kipindi hiki cha mgomo, wagonjwa waliofariki wanaweza
kufikia 25.

MBEYA
Mwandishi wetu wa Mbeya, Gordon Kalulunga,
anaripoti kuwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoani humo wagonjwa
wanaofikia 22 walipoteza maisha na wengine walitoroshwa na ndugu zao
wakiwa na dripu baada ya kuona hali zao ni mbaya.

DODOMA
Mwandishi
wetu Dodoma anaripoti kuwa mgomo huo umesababidha adha kubwa kwa
wagonjwa na inakadiriwa watu tisa wamefariki dunia huku wengi
wakirudishwa majumbani kwao.

MOROGORO
Mwandishi wetu, Dunstan Shekidele anaripoti:
Kwa
mujibu wa mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa
wa Morogoro aliyeomba jina lake lihifadhiwe, watu wanaokadiriwa 14
wamefariki dunia tangu mgomo huo ulipoanza.
“Kuna baadhi ya ndugu
wamewaondoa wangonjwa wao wakiwa na dripu, kwa kweli hali ni mbaya,
tumeambiwa wengine wanafia majumbani,” alisema mhudumu huyo.

KIGOMA, IRINGA NA TANGA
Waandishi wetu katika mikoa hiyo wameripoti vifo idadi yake katika mabano kama ifuatavyo;
Kigoma (nane), Bombo mkoani Tanga (nane) na Iringa (saba).
Hata
hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda ilikuwa akutane na madaktari
Jumapili iliyopita kuzungumzia mgogoro huo lakini ikashindikana kwani
Mwenyekiti wa Madaktari, Ulimboka Stephen aliliambia gazeti hili kuwa
Ofisi ya Waziri Mkuu ilichelewesha barua ya mwaliko.
Madaktari hao
wameitisha mgomo wakidai kuongezewa posho ya kufanya kazi katika
mazingira magumu hatarishi , nyumba na usafiri wa kwenda na kurudi
kazini.SOURCE: GLOBAL PUBLISHERS TZ

No comments: