Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umeanza zoezi la kuwarejeshea nauli zao wasafiri wapatao 1920 ambao walikuwa wasafiri na treni kutoka Dar kwenda Kigoma siku za Jumamosi Jan 07, 2012 na Jumanne Jan 10, 2012 ambazo zimelazimika kufutwa baada ya reli ya kati kuharibika.
Zoezi hili limechelewa kutokana na siku ilipotokea dharura ya kuahirishwa ilikuwa ni alasiri Jumamosi Januari 07, 2012 na hivyo utawala wa TRL ulishindwa kupata fedha za kuwarejeshea kwa wakati kwa vile siku iliyofuata ilikuwa Jumapili ambapo huduma za benki zinakuwa hazipo.
Wakati waraka huu ukitumwa zoezi la kurejesha nauli linaendelea katika stesheni ya Dar es Salaam kwa utulivu.
Uongozi unasisitiza kuwa uamuzi wa kuanza tena huduma ya abiria ulichukuliwa siku ya Jumatano Januari 4, 2012 kwa nia njema kwa vile ukarabati ulikuwa umekamilika, hata hivyo bila ya kutarajia kwa mapenzi ya Mungu m,vua nyingi zilinyesha na mafuriko yalitokea tena siku ya Jumamosi Januari 07, 2012.
Aidha kuhusu lini huduma itarekeshwa tena itategemea jinsi hali ya mvua ikitengemaa na kuwa za kawaida kwani eneo la tukio kuna wahandisi na mafundi wanaofanya kazi ya kukarabati eneo korofi kwa mafuriko la Godegode mkoani Dodoma kwa saa 24! mafanikio ya kazi hiyo itategemea kama mvua zitakuwa za wastani na si za mfululizo kama sasa.
TRL kila siku uchao inapoteza mapato kwa wastani Shs milioni 81.3 kwa treni za mizigo na shs milioni 59 kwa safari nne za abiria ambazo zimefutwa kila wiki.
Katika wakati huu mgumu Uongozi wa TRL unaomba ushirikiano wa Wananchi wa jumla hasa maeneo ya reli ya kati inamopita nchini kutoa taarifa waonapo uharibifu wa aina yeyote katika mamlaka zilizo karibu nayo ili hatua za kiusalama zichukuliwe.
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano ya TRL kwa Niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi K.A.M.Kisamfu.
Imesainiwa:
MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO
TRL MAKAO MAKUU
DAR ES SALAAM.
JANUARI 09, 2012
No comments:
Post a Comment