Friday, January 20, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - KIFO CHA MAREHEMU JEREMIAH SUMARI

Marehemu Jeremiah Sumari

Kwa masikitiko Makubwa, Ofisi ya Bunge inawatangazia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kuwa aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo tarehe 19 Januari, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia na Chama chake imeandaa shughuli ya kuaga rasmi mwili wa Marehemu siku ya Jumamosi, tarehe 21 Januari, 2012 katika Viwanja vya Karimjee kuanzia saa 5 asubuhi na baada ya hapo atasafirishwa siku ya Jumapili asubihi kuelekea Kijijini kwao Akeri, Meru, Mkoani Arusha kwa mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatatu tarehe 23 Januari, 2012.

Kutokana na msiba huo, shughuli za Kamati kwa siku za Jumamosi tarehe 21 Januari, 2012 na Jumatatu tarehe 23 Januari, 2012 zimesitishwa na zitaendelea tena siku ya Jumanne tarehe 24 Januari,2012 baada ya maziko.

Marehemu alikuwa anaumwa Saratani ya Ubongo ambayo ilimsumbua kwa muda mrefu na mnamo mwaka 2010 alipelekwa nchini India kwa upasuaji na alirejea nchini na hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri. Hata hivyo mwishoni mwaka 2011 hali yake ilibadilika ghafla na kuanza kuwa mbaya alirejea nchini tarehe 9 Januari, 2012 na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alifariki dunia tarehe 19 Januari, 2012.
Marehemu ameacha mjane na watoto wanne (4).

MWENYEZI MUNGU AIWEKE ROHO YA MAREHEMU
MAHALI PEMA PEPONI, AMEN
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
S. L. P. 9133
DAR ES SALAAM
19 Januari, 2012

No comments: