Wednesday, January 11, 2012

Kafulila atiwa mbaroni kigomaAnthony Kayanda, Kigoma
POLISI mkoani Kigoma wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha NCCR Mageuzi waliokuwa kwenye mkutano ambao ulipaswa kuhutubiwa na mbunge Kigoma Kusini, David Kafulila.

Habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Kazuramimba ambako Kafulila alikuwa amejiandaa kufanya mkutano wa hadhara na tayari alikuwa ameanza kuhutubia akiwa kwenye gari na madiwani wawili wa chama hicho cha upinzani.

Kafulila aliliambia gazeti hili jana kuwa polisi hao walizuia mkutano wake na kumkamata kwa mahojiano yaliyodumu kwa takriban dakika 30, kwa madai kwamba mkutano wake haukufuata taratibu za kuomba na kupata kibali.

Kafulila ambaye yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kichama, alisema alipofika kijijini hapo alipata taarifa kwamba polisi wa kituo kidogo kilichopo eneo hilo waliwazuia viongozi wa NCCR Mageuzi kufanya maandalizi ya mkutano huo.

Alisema baada ya kusikia uamuzi huo, alilazimisha wafanye mkutano kwa vile yeye ni mbunge halali wa jimbo hilo la Kigoma Kusini na anapaswa kuzungumza na wananchi kuelezea utendaji wake wa kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

“Polisi wamenizuia kufanya mkutano wangu na wametumia nguvu kubwa kututawanya kwa madai kwamba wametumwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kigoma (OCD), Japhet Kibona eti sisi hatujatimiza masharti..., na pia hatujaomba kibali cha kufanya mkutano. Sasa mimi kama mbunge wa jimbo nazuiliwa kwa nini?," alihoji Kafulila na kuendelea:

"Inawezekana huyu OCD ananihujumu na tayari nimewaeleza wakuu wake wa kazi kuanzia IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha ili wajue hujuma ninayofanyiwa na huyu OCD wa Kigoma,"alisisitiza Kafulila..soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments: