Monday, January 16, 2012

Wanasheria wafungua kesi kupinga Mchakato wa Katiba



Fredy Azzah




CHAMA
cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimewateua mawakili wanne
watakaosimamia kesi ya kupinga sheria ya kuundwa kwa katiba mpya
iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana.

Rais wa chama hicho, Francis Stolla, aliliambia gazeti hili jana
kuwa Mawakili hao ni pamoja na Profesa Gamalieli Simbo, Wakili
Richard Rweyogeza, Silwami Gallapi Mwautembe pamoja na Fulgence Massawe.

“Tumewapa
na hadidu za rejea, moja ni kuhakikisha kuwa hii kesi inafunguliwa
kabla ya huu mwezi kwisha,” alisema Stolla.Alisema kuwa, majukumu
mengine ya mawakili hao ni kufanya utafiti juu ya kesi hiyo na kuandika
mashtaka pamoja na kuisimamia kesi hiyo.

“Kesi ikiisha itabidi pia waje kutoa ripoti katika chama,” alisema Stolla.
Alieleza kuwa, mawakili hao wataisimamia kesi hiyo bila kupewa malipo yoyote na chama hicho kwa kuwa na wao ni wanachama.

“Gharama
ambazo chama kitatoa ni zile za ada ya kufungua kesi pamoja na kutoa
fotokopi za nakala mbalimbali,” alieleza Stolla. Aliongeza kuwa, kwa
kuwa kesi hii ni ya kikatiba chama hicho hakitatoa notisi kwa serikali
kabla ya kuifungua.






"Hii ni kesi ya kikatiba, haihitaji kutoa taarifa kwa Serikali.Tunatumia sheria ya haki za msingi na wajibu wa kutekeleza ya mwaka1994," alisema Kwa mujibu wa Stolla, kesi hiyo ni dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.

“Tumeunda kamati ya kushughulikia katiba, yenye wajumbe wanane.
Kwa sasa wajumbe hao wako katika mchakato wa kuandaa hati ya mashtaka.
Wakimaliza, tutateua mawakili watatu wa kuisimamia kesi hiyo
mahakamani kwa niaba ya chama,” alisema Stolla.




“Kwa sababu sheria inasema ukitaka kiishtaki serikali inabidiumshitaki Mwanasheria Mkuu, kwa hiyo tutafanya hivyo lakini kesi hii niya kikatiba na mlengwa wetu ni Bunge,” alisisitiza. Alisema hatua ya
kulishtaki inatokana na dhamana ya chombo hicho ya kutunga sheria.
"Tunalishtaki kwa sababu sheria hiyo iliyoitunga ni mbovu,” alisema.

Stolla alisema sababu za kufungua shtaka hilo ni pamoja na sheria
hiyo kukiuka katiba ya Tanzania ya mwaka 1977. Alitaja ibara
zilizokiukwa kuwa ni pamoja na ile ya 18 inayowapa nafasi wananchi
kutoa maoni yao na ibara ya 22, inayotaka wananchi washirikishwe kwenye
masuala muhimu na yenye maslahi kwao.

Kwa mujibu wa Stolla sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo, nisheria hiyo kukiuka taratibu za utungwaji wa sheria, ikiwa ni pamoja nakupitishwa na Bunge baada ya kusomwa mara mbili, badala ya mara tatu
kama inavyotakiwa kisheria. “Mara ya kwanza walipowasilisha hati ya
dharura bungeni, kelele zilipigwa kuwa iondolewe na utaratibu wa
kutungwa kwa sheria hii uwe wa kawaida. Pia kutaka ule muswada uandikwe
kwa lugha ya Kiswahili, mambo yale yalitekelezwa,” alisema.

Alisema kuwa baada ya kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo
Watanzania wengi wanaielewa, muswada ulipaswa kurudishwa kwa wananchi
ili waujadili lakini jambo hilo halikufanyika. “Siku ile wanasoma ule
muswada wa Kiingereza kwa mara pili, waliusoma ule wa Kiswahili kwa
mara ya kwanza lakini wakadai kuwa ni mara pili. Halafu wakaja kusoma
tena mara ya pili na kuupitisha.

Sheria inataka usomwe mara tatu, kwa hiyo ni wazi kuwa huuulipitishwa baada ya kusomwa mara mbili badala ya mara tatu kamainavyotakiwa,” alifafanua Stolla. Alisema sababu nyingine ni sheria
hiyo kuwa na vipengele vinavyozuia watu au asasi nyingine nje ya tume
itakayoundwa kuwaelimisha wananchi juu ya katiba.

Stolla alisema katika kifungu cha 22, sheria hiyo inaweka makosa ya
jinai na adhabu kwa mtu ama taasisi, itakayofanya kampeni ya
kuhamasisha juu ya katiba. “Kwa sheria hii midahalo kama inayofanywa
sasa hivi inaharamishwa, ni tume ya katiba mpya tu ndiyo itahamasisha
kwa mikutano maalumu, kwa hiyo sisi tunadhani kuwa hali hiyo inanyima
uhuru wa kutoa maoni,” alieleza.




No comments: