Thursday, January 26, 2012

WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa Anna Tibaijuka:“Hivi Kweli Unafikiri inawezekana Nikakurupuka Nikaenda Kuomba Eneo Bila Rais Jakaya Kikwete Kujua?Atakayejaribu Kunikomoa Atajikomoa Yeye MwenyeweWaziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya Andiko la Serikali kwenda jumuia za Kimataifa kudai kuongezewa sehemu ya bahari. Waziri Tibaijuka aliamua kutolea ufafanuzi huo hii jana jijini Dar es Salaam baada ya kuibuka kwa mijadala juu ya mpango huo.
Waziri Prof. Tibaijuka akizungumza na wana habari hii Jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Selassie Mayunga
---
Na Hellen Mlacky
-
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema hakukurupuka kwenda kuomba Tanzania iongezewe eneo la ziada la maili 150 nje ya Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilishirikishwa kikamilifu.

“Hivi kweli unafikiri inawezekana nikakurupuka nikaenda kuomba eneo bila Rais Jakaya Kikwete kujua? Atakayejaribu kunikomoa atajikomoa yeye mwenyewe, mimi sijui ni kwa nini tunagombea fito wakati tunajenga nyumba moja,” alisema Profesa Tibaijuka.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Profesa Tibaijuka alisema madai ya Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu (CUF) kwamba SMZ haikushiriki hayaendani na yaliyojiri kwa kuwa wajumbe na viongozi kutoka Zanzibar wameshiriki na kufanyia kazi andiko hilo kwa bidii.

Aliwataja wajumbe walioteuliwa katika kamati mbalimbali kutoka SMZ kuwa ni Mwalimu A. Mwalimu aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati, Ujenzi na Makazi ambaye alikuwa mjumbe katika Kamati ya Makatibu Wakuu.

Katika Kamati ya Ufundi, aliteuliwa Haji Adam Haji aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa SMZ, ambaye alishiriki kikamilifu kama Mwenyekiti Kamati ya Ufundi na wakati wa kupima alama za mpaka Januari 2011, kikosi kazi kutokaTanzania Bara kilishirikiana na wataalamu wapimaji kutoka SMZ kukamilisha kazi hiyo.

“Upimaji huu ulifanyika chini ya usimamizi wa Masheha wa Kiuyu, Maziwa Ng’ombe, Kojani na vitongoji kwa upande wa Kisiwa cha Pemba na Makunduchi kwa upande wa Kisiwa cha Unguja. Pia Omar Zubeir aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati,” alisema.

Alisema katika Kamati ya Utekelezaji, Pandu Makame kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikosi kazi cha mradi huo na baadaye andiko liliwasilishwa Umoja wa Mataifa, New York Marekani Januari 18 ambapo aliongozana na viongozi na wataalam kumi wakiwemo wajumbe wawili kutoka SMZ.

“Shamhuna (Ali Juma), Waziri wa Ardhi, Maliasili na Nishati, hakuhudhuria lakini alimteua Ayoub Mohamed Mahmoud, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara yake kumuwakilisha ambapo alishiriki kikamilifu na kupewa nafasi kuongea kwa niaba ya SMZ,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alisema pia Spika wa Bunge alialikwa kuteua wabunge wawili katika ziara hiyo ambapo Abdulrahman Hassan Shah Mbunge wa Mafia, aliwakilisha Tanzania Bara na Zhakia Meghji aliwakilisha Zanzibar.

Kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Zanzibar Mohamed Juma Omary, alishindwa kusafiri dakika za mwisho kutokana na dharura iliyojitokeza.

Jussa hivi wiki hii aliwasilisha hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi kupinga Tanzania isipewe eneo hilo kwa madai Zanzibar haikushirikishwa.


No comments: