Thursday, February 9, 2012

Kilaini: Mgomo wenu madaktari ni maafa kwetu


Waandishi Wetu
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodus Kilaini amewasihi madaktari kuangalia upya uwezekano wa kudai maslahi yao kwa njia mbadala na mgomo ambao unasababisha maafa.

Akizungumza na Mwananchi, Askofu Kilaini alisema pamoja na madaktari kuwa wana hoja katika madai yao, hakubaliani na mgomo kwa kuwa ni kinyume na maadili.

Askofu Kilaini alisema, “Madaktari ni watu muhimu zaidi na iwapo ingeitishwa kura ya kubainisha nani alipwe zaidi kati ya madaktari na wabunge, watu wengi wangependekeza walipwe zaidi madaktari na siyo wabunge," alisema Kilaini na kuongeza:

"Lakini mimi sikubaliani na jinsi wanavyogoma na kupita hospitali huku wameweka mkono mfukoni na kuacha watu wakiwa wamejilaza pembeni wanaumwa.”

Alisema japokuwa malipo wanayolipwa ni kidogo na yanakatisha tamaa, madaktari wanapaswa kuwa na huruma na wananchi ambao wamekuwa wakitaabika kwa kukosa tiba kutokana na mgomo huo.

Muhimbili bado

Katika hospitali za Muhimbili na Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), wagonjwa waliolazwa katika wodi mbalimbali wameomba serikali kushughulikia suala hilo kama ilivyo kwa masuala mengine ya dharura.

Wakizungumza kwa uchungu katika wodi ya Sewahaji, walisema kinachoendelea mgomo huo sasa ni janga linalohatarisha maisha yao na ya ndugu zao.

Janne Shaban ambaye alidai amefika hosptalini hapo kumuuguza mumewe, alisema kitendo cha serikali kushindwa kutatua tatizo la madaktari ni hatari na kitaangamiza maisha ya watu wengi wasio na hatia.

"Mimi nipo nimekuja na mume wangu amelazwa katika wodi ya Sewahaji, mgonjwa anaumwa hapati tiba na sasa tumeambiwa tuondoke tuende wapi? Nyumbani kunanini cha kumpa mgonjwa? alihoji Shabani na kuongez: serikali inapaswa kulichukulia tatizo hilo kama janga la dhararu kwani linahatarisha maisha ya walio wengi.

Hata hivyo, Msemaji Mwandamizi wa Hospitali hiyo Aminiel Aligaesha alisema uongozi wa hospitali hiyo umepokea barua kutoka kwa madaktari hao bingwa unaoelezea azima ya mgoma huo.

Alisema kutokana na hatua hiyo huduma katika hosptali hiyo zitaendelea kuzorota huku akisisityiza kuwa idadi ndogo ya madaktari bingwa itaendelea kufanya kazi ya kuangalia wagonjw akatika kitengo cha dhararu.

Mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari inayoongoza harakati za mgomo huo, Dk Stephen Ulimboka alisema madaktari wataendelea na mgomo hadi madai yao yatakapotekelezwa.

Mgomo Bugando

Madaktari waliopo katika mafunzo ya vitendo wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), jijini Mwanza wametangaza kuanza mgomo rasmi kuanzia jana saa 6:00 mchana na kuungana na madaktari bingwa wa hospitali ya Muhimbili walionza mgomo juzi.

Hatua hiyo itasababisha madaktari bingwa wa Bugando walioajiriwa na kanisa Katoliki kushindwa kutoa huduma, tofauti na hapo awali ambako madaktari wa mafunzo kwa vitendo, ndiyo wanaopaswa kuwapokea wagonjwa na kuwahudumia kabla ya kufika kwa madaktari bigwa.

“Iwapo madaktari walio katika vitendo watatekeleza azma yao ya kugoma, itatubidi sisi madaktari bigwa tuanze kuhudumia wagonjwa kwa masaa ishirini na nne jambo ambalo litakuwa gumu kwetu na tutashindwa kufanya kazi,”alisema mmoja wa madaktari bingwa ambaye hakutaka jina lake kutajwa .

Alisema madaktari bingwa ni wachache kulingana na wagonjwa wanaopokelewa hospitalini hapo na kusema, wanahofia hali ya matibabu BMC itakuwa ngumu kulinganishwa na hapo awali.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa hospital hiyo Dk Japhet Ngilioma alisema siyo rahisi kilichotokea katika hospital ya Muhimbili kutokea katika hospitali hiyo ya Bugando kutoka na hospitali hiyo kuwa chini ya uangalizi wa kanisa Katoliki.

Alisema hadi saa 6:00 mchana madaktari wote bingwa waliokuwepo katika zamu walikuwa kazini na kliniki zote zilikuwa zikifanya kazi bila ya kuwepo dalili yeyote ya mgomo kwa madaktari wa pande zote mbili.

No comments: