Thursday, February 23, 2012

TLP, Sau Tayari Arumeru


[Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Paul Kyara (kushoto), akimpongeza mgombea wa kiti cha ubunge kupitia tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Shaaban Kirita, mara baada ya kumtangaza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Katibu Uenezi wa chama hicho, Johnson Mwangosi. Picha na Joseph Zablon. ]

Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Paul Kyara (kushoto), akimpongeza mgombea wa kiti cha ubunge kupitia tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Shaaban Kirita, mara baada ya kumtangaza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Katibu Uenezi wa chama hicho, Johnson Mwangosi. Picha na Joseph Zablon.
Waandishi Wetu
WAKATI Kamati Kuu ya Chadema inatarajiwa kukutana Machi 3, mwaka huu kumpitisha Mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki, Chama cha Tanzania Labour (TLP) na Sauti ya Umma (Sau), vimetangaza wagombea wao kwenye kinyang’anyiro hicho.

Kamati Kuu ya Chama cha Sau, katika kikao chake kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, kilimtangaza Shaaban Kirita na TLP wamemsimamisha Abraham Chipaka.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Uenezi wa Sau, Johnson Mwangosi, alisema uamuzi wa kumsimamisha Kirita kuwania nafasi hiyo, umefikiwa katika kikao cha kamati kuu kilichofanyika Jumamosi iliyopita.

“Tunamsimamisha Kirita ambaye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la chama chetu,” alisema Mwangosi na kwamba, amepata nafasi hiyo baada ya kuwashinda wanachama wengine ambao ni Mohamed Mgate na Susan Maro.
Alisema Kirita amechaguliwa kutokana na mchuano mkali uliokuwapo baina ya wagombea ambao wana vigezo, ambavyo vinakaribiana na baada ya vuta nikuvute hatimaye wajumbe walipitisha jina lake.

Mwangosi alisema mgombea huyo ni mpambanaji msomi, mfanyabiashara na ana uzoefu wa kutosha katika masuala ya siasa na uchaguzi na kwamba, alikuwa ‘mwiba mkali’ kwa wanaharakati wa vyama vingine vya siasa uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga.

Alisema wanampeleka Kirita Arumeru Mashariki kutwaa kiti siyo kushiriki uchaguzi, kwa sababu mgombea huyo ni mwenyeji na anazijua changamoto zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Katika tukio lingine, Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Arusha, Leonard Makanzo, alisema Abraham Chipaka alipatikana baada ya kumshinda katika kura za maoni, Fanuel Palangyo.
“Wajumbe wa mkutano wa jimbo walimchagua Chipaka hivyo kamati yetu ya utendaji mkoa pia imempitisha,” alisema Makanzo.

Makanzo alisema ili kuhakikisha upinzani unashinda kiti hicho, wanaomba Chadema wawaunge mkono kama walivyofanya wao Jimbo la Igunga.“Tuliwaachia Igunga sasa tunaomba watuachie Arumeru na watuunge mkono ili tuing'oe CCM,” alisema Makanzo.

Chadema wachukua fomu
Katibu wa Chadema Jimbo la Arumeru Mashariki, Totinan Ndonde, alisema hadi jana ni wanachama sita waliokuwa wamechukua fomu na hakuna alikuwa amerejesha.

Ndonde alisema kikao cha kamati kuu, kitatanguliwa na Mkutano wa Baraza Kuu Chadema katika jimbo hilo, Kamati ya Utendaji Wilaya ya Arumeru na Sekretarieti ya chama wilaya.

“Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Februari 25, tunatarajia mgombea wetu atajulikana Mach 3, baada ya kikao cha kamati kuu,” alisema Ndonde.Alisema waliochukua fomu hadi jana ni Joshua Nasari, Godlove Temba, Yohane Kimuto, Rebecca Mugwisha, Samwel Shami na Anna Mughwira.

Walioshindwa CCM wasubiri
huruma ya vikao vya juu.
Waliokuwa wanawania kuteuliwa na CCM kuwania ubunge Arumeru Mashariki na kubwagwa na Sioi Sumari, mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremiah Sumari, wameeleza kusubiri uamuzi wa vikao vya juu.
Wakizungumza baada kinyang'anyiro cha kura za maoni, baadhi ya wagombea hao, walisema kilichotokea katika upigaji kura kimeonekana na wao wanasubiri chama hicho kutoa uamuzi.

Elirehema Kaaya, ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Nyangamana, mkoani Mwanza, alisema zoezi la kura za maoni limekwisha na sasa wanasubiri uamuzi wa chama.

“Sina maoni kama unavyojua kura za maoni ni hatua za mwanzo za mchakato, nadhani tusubiri uamuzi wa vikao vya juu,” alisema Kaaya ambaye alishika nafasi ya tatu kwa kura 205.

Maoni hayo ya Kaaya yalionekana kuungwa mkono na wagombea wengine, walioangushwa na Sumari aliyepata kura 316, akifuatiwa na William Sarakikya (259), Elishiria Kaaya ambaye ni mjumbe wa Nec (176), Anthony Musari (22) na Moses Urio (11).

Mgogoro CCM
Viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Arusha, wametaka viongozi wa juu wa CCM kuwakemea tena wenzao mkoani hapa wenye njama za kumdhoofisha kisiasa Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige.Soma zaidi www.mwananchi.co.tz

No comments: