Tuesday, February 28, 2012

Wabunge wamkana Spika Anne Makinda

Spika, Anne Makinda
Baadhi ya wabunge wa Bunge, wamesema uongozi wa umma sio fedha pekee na kwamba hawana mpango wa kuachana na siasa kutokana na kulipwa mshahara na posho kidogo.

Walitoa kauli hiyo walipozungumza na NIPASHE, kufuatia kauli ya Spika, Anne Makinda, kuwa nusu ya wabunge hivi sasa wanatamani kuachana na siasa na kwenda kufanya walizosomea kutokana na kulipwa mshahara mdogo pamoja na posho.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema uongozi sio fedha na kwamba kama mbunge alitaka kuingia bungeni kwa ajili ya kupata utajiri anaweza kuona kazi hiyo kwa sasa haifai na kukiri kwamba mshahara wanaopata wabunge hauotoshi ikilinganishwa na mahitaji ya wananachi wanaowawakilisha, lakini hiyo sio sababu ya kutosha.


Alisema kitu cha kwanza wanachoangalia kwa wabunge makini ni kuwawakilisha wale waliowachagua na kwamba fedha kinakuwa kitu cha mwisho katika kufikiria badala ya kukitanguliza.
Alisisitiza kuwa uongozi ni dira na wala fedha haina nafasi yoyote kwa kiongozi makini kama mbunge na kwamba mtu anayetaka ubunge ili awe tajiri hafai kuchaguliwa.
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndasa, alisema wabunge hawakuchaguliwa kwa lengo la kwenda kupata mshahara mnono badala walipewa jukumu hilo ili kuwatumikia wananchi.
Alisema mbunge makini hawezi kutegemea mshahara na posho pekee na badala yake anatakiwa kufanya kazi zingine za ujasiliamali ili kujiingizia kipato.
“Nilitaka kwenda bungeni ili kuwawakilisha wananchi na sio kutafuta utajiri hivyo sioni shida yoyote mpaka nitamani kuachana na siasa eti kutokana na posho ndogo au mshahara mdogo kama alivyosema Spika,” alisema.
Mbunge wa Serengeti (CCM), Dk. Kebwe Stephen Kebwe,, alisema hana mpango wowote wa kuachana na siasa kutokana na kipato kidogo na badala yake ataendelea kuwawakilisha wananchi wake kama kawaida.
Alisema alipoomba nafasi hiyo mwaka 2010 aliwaambia wananchi wamchague ili awawakilishe bungeni, lakini sio wamchague ili akapate utajiri kupitia mishahara na posho nono.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margareth Sitta, alisema kuna haja ya kumuuliza Spika Makinda ili aeleze alikopata takwimu kwamba nusu ya wabunge wanatamani kuachana na nafasi zao na kwenda kufanya kazi walizosomea.
“Mimi sina takwimu manake isije ikawa Spika alizungumza na wabunge wawili halafu akasema nusu ya wabunge wanatamani kuachana na ubunge kutokana na posho na mshahara mdogo,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alisema hana uhakika kama kweli wabunge wametaka kujiuzulu kutokana na kulipwa kidogo.
Alisema kama kuna watu wanawaza hivyo hao sio wabunge na kwamba walipaswa kujiondoa muda mrefu kwa kuwa hawafai kuwawakilisha wananchi.
Mbunge wa Karatu (Chadema), Israel Natse alisema wabunge wa CCM ndio wanaotamani kujiuzuru, lakini kwa upande wa upinzani hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa wao sio wabunge wa posho na kwamba wanajali kwanza kuwatumikia wananchi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: