Friday, March 9, 2012

NHIF; Tutaongeza wigo wa wanachamaNa Mwandishi Wetu, Manyara

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kuwa utahakikisha unaongeza wigo wa wanachama kwa kuimarisha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kutimiza lengo lake la kufikia asilimia 30 ya Watanzania kuwa kwenye utaratibu wa Bima ya Afya ifikapo 2015.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Fedha Mipango na Uwekezaji Bw. Deudedit Rutazaa wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya tangu uanzishwe mwaka 2001 kwa wadau wa Mfuko huo mkoani Manyara.

Alisema kuwa ili kufikia lengo hilo, Mfuko utavihusisha Vikundi mbalimbali, vyama vya Ushirika, shule na vingine lakini pia kuishauri Serikali kubadili sheria iliyopo.

"Tutaendelea kuwekeza katika miradi ya uboreshaji wa huduma za afya kwa kuwa na vituo vya mifano katika mikoa mingine hususan iliyoko pembezoni, tutaimarisha utendaji wa Mfuko kwa kusogeza zaidi huduma kwa wanachama wetu hasa kufungua ofisi kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 na kupanua zaidi wigo wa huduma kwa wanachama wetu kwa kuwawezesha kupata huduma ndani ya Afrika Mashariki," alisema Rutazaa.

Alisema kuwa ili hayo yaweze kufanikiwa ni vyema sasa wadau wote wakaelewa haki na wajibu wao katika Mfuko ili waweze kuelimisha wananchi wengine kujiunga na Mifuko ya NHIF na CHF.
"Jambo jingine tungewaomba sana viongozi kusimamia matumizi ya fedha ambapo sisi kama Mfuko tutatoa taarifa za utekelezaji kwenye uongozi wa Mkoa na Wilaya kila robo ya mwaka na kuziwasilisha katika Baraza la Madiwani, fedha hizi zikitumika vizuri zitachangia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma kwa wanachama wetu na kwa wananchi kwa ujumla," alisema Rutazaa.

Hata hivyo wakati akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bw. Erasto Mbwiro alizitaka Halmashauri kuangalia uwezekano wa kuwa na sheria zitakazowalazimisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ili wawe na uhakika wa matibabu wakati wowote.

Alisema kuwa Mfuko huo wa Afya ya Jamii hauwezi kuwa na mafanikio ya kutosha endapo hapatakuwa na sheria inayomlazimisha mwananchi kujiunga nao hivyo akawataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuliangalia hilo kwa makini ili liweze kufanikiwa.

"Hakuna mtu anayependa kuumwa na ugonjwa unakuja wakati ambao hata hela hauna hivyo ni lazima huu Mfuko tuuchangamkie ili wananchi wetu wapate uhakika wa matibabu ...bila afya njema hakuna maendeleo na maadui umasikini na ujinga ndiyo yatapata nafasi," alisema Mbwiro.
Pia alizitaka Kamati za Afya na Elimu kuhakikisha zinafanya kazi ya kuwaelimisha wananchi kuhusiana na Mfuko huu ili wajue faida zake na wahamasike kujiunga nao.

"Haiwezekani Manyara tukawa kwenye asilimia tatu ya kaya zote zilizoko mkoani hapa na wakati kila kaya ina mifugo ya Ng'ombe na kuku...na mchango wa Mfuko huu ni kati ya elfu kumi au shirini ambazo zinaweza kutokana na kuuza hata kuku mmoja tu hivyo ni lazima tujipange,' alisema Mkuu huyo.

No comments: