Saturday, April 14, 2012

Liyumba alikiri kukutwa na simu gerezani -Shahidi

 

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, amekiri kukutwa na simu na kuomba asamehewe baada ya jaribio lake la kutaka kuitumbukiza chooni kushindikana.
Hayo yalisemwa na shahidi namba mbili B 4948 WDR Patrick ambaye pia ni Askari Magereza katika kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili mshatakiwa Liyumba kipindi alipokuwa mfungwa kwenye gereza la Ukonga.
Akitoa ushahidi wake, mbele ya Hakimu Mkazi, Stuart Sanga, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Patrick alidai kuwa,  kabla ya mshtakiwa huyo hajafanikiwa kutumbukiza simu hiyo chooni alifanikiwa kuipora.

Liyumba ambaye wakati huo alikuwa ni mfungwa mwenye Na.303/2010, anadaiwa kuwa Julai, mwaka 2011, ndani ya Gereza la Ukonga, alikutwa na simu ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye Na. 0653-004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa akiitumia kufanyia mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria.
Akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Elizabeth Kaganda, Patrick alidai kuwa, siku ya tukio alipewa taarifa na mfungwa mmoja ambaye ni Nyapara Hamidu Enja kuwa alimuona mfungwa mwenye chumba namba 9, Liyumba akiwa anaongea na simu.
Alidai kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alienda kwa mwendo wa kunyata hadi dirishani hapo na kumuona Liyumba akiwa amekaa kwenye ndoo kwa kugeukia kitanda chake, huku akiwa amevalia miwani na mkononi mwake alikuwa ameshikilia mkebe wa miwani wenye rangi ya bluu ambao ndani yake ukiwa na simu aliyokuwa akiibonyeza kwa kutumia kalamu.
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa,  alimchunguza kwa muda wa dakika mbili kabla ya kuamua kuufungua mlango huo kwa kushtukiza, kitendo kilichosababisha kushtuka na kutaka kuitumbukiza simu hiyo chooni lakini alimuwahi na kuipora kabla hajafanya hivyo.
Patrick alidai kuwa, baada ya kumkamata walishauriana na WDR Iman na kuamua kumpeleka kwenye ofisi ya usalama ambapo huko walimkuta SP John Vulva, Inspekta Makongele, Inspekta Mwakusya, Inspekta msaidizi Tairo na ASP Nyamka na alipohojiwa alikiri kosa na kuomba msamaha.

Alidai kuwa, baadaye askari Vuliva aliyekuwa akiwaongoza askari hao aliamuru Liyumba apelekwe kwa mkuu wa gereza.
Patrick alidai kuwa, baada ya kufikishwa kwa mkuu wa gereza, Liyumba aliulizwa mahali alipoipata simu hiyo ambapo kwa kauli yake kwa mara nyingine alidai presha imepanda tena na kuomba karatasi ili aandike ambapo katika maelezo yake alikiri kosa na kuomba msamaha huku akisema kuwa simu hiyo aliiokota nyuma ya simtenki ndani ya gereza hilo.

Shahidi namba moja ambaye ni mfungwa mwenye namba MF 891/1999, Hamidu Henji, alidai mahakamani hapo kuwa, wakati Liyumba akihojiwa na uongozi wa gereza hilo, yeye alikuwa nje.
Henji ambaye ni Nyampala aliyaeleza hayo jana wakati alipokuwa akihojiwa na wakili wa Liyumba, Majura Magafu mara baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake.
Akihojiwa na Wakili Magafu aliulizwa kuwa kilichoandikwa kwenye maelezo yake ya onyo kuwa aliwaoongoza askari kumhoji Liyumba awaeleze simu aliipata wapi, alifanya hivyo au la? Alidai kuwa yeye alikuwa nje na hakumuhoji na wala hajui wakati anahojiwa alikuwa anajibu nini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: