Saturday, April 14, 2012

Maggid Mjengwa: Siku Nilipomsikia Nyerere Akilitangazia Taifa Kifo Cha Sokoine

Ndugu zangu,



KUNA wengi  tunaokumbuka tulikuwa wapi siku
ile ya tarehe 12 Aprili, 1984 wakati Mwalimu Nyerere alipolitangazia
taifa kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine kilichotokana na ajali ya
gari eneo la Wami-Dakawa  akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar.



Kwa bahati mbaya, vijana wengi waliozaliwa baada ya 1984 hawajui sana habari za Edward Moringe Sokoine . Mimi
nilikuwa Kidato cha Pili tu pale Sekondari ya Tambaza. Nakumbua ilikuwa
majira ya saa kumi jioni.  Nilikuwa natembea kwa miguu kutoka Kinondoni
’ A’ kuelekea nyumbani Kinondoni Biafra. Nilipofika maeneo ya jirani na
Msikiti wa Mtambani nikasikia wimbo wa taifa unapigwa.



Nilihisi haraka kuna jambo
kubwa la kitaifa limetokea. Nikasogea kwenye duka la jirani. Wapita njia
wengine nao walisogea mahali hapo. Wimbo wa Taifa ulipomalizika,
nikamsikia Mwalimu akianza kutamka kwa sauti ya huzuni; ” Ndugu
Wananchi, leo hii…” Kilichofuata ni historia ambayo hapa nashiriki
kuiandika.



Naam, Sokoine alikuwa
kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma. Ni Sokoine
aliyetufanya hata tuliokuwa sekondari  wakati huo, tuwe na imani na
uongozi wa nchi. Tuwe na matumaini ya maisha bora kwa siku za baadae.
Ndio, ukitoka kwa Mwalimu,
ni Sokoine pia aliyechangia katika kutufanya watoto wa wakati huo,
tuamini na tuipende siasa. Alikuwa mfano wa kuigwa. Alishi kama
alivyohubiri. Siyo tu hakujilimbikizia mali, halipunguza hata mali zake
ili apate nafasi zaidi ya kututumikia Watanzania.

Itakumbukuwa,
kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili, 1984, Sokoine alikabiliana n
ahoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao. Sokoine
alitamka;



”  Ndugu Spika, niko tayari
kuwaongezea wabunge posho ya chakula chao, lakini kamwe sitakuwa tayari
kuwaongezea mishahara na marupurupu mengine.” Mwisho wa kunukuu. Huyo
ndiye Edward Moringe Sokoine.  Alikuwa kiongozi wa kanuni na mwenye
msimamo usioyumba.



Sokoine alielewa, kuwa
ukiwalinganisha na wananchi walio wengi, wabunge walikuwa na hali bora
zaidi kimaisha. Alikuwa tayari kuchukiwa na wabunge kwa kutetea maslahi
ya wanyonge, kuliko kupendwa na wabunge kwa kujali zaidi maslahi yao. 



Baada ya kikao kile cha
Bunge, Edward Sokoine, badala ya kupanda ndege ya Serikali kumrudisha
Dar es Salaam, aliamua kurudi Dar Es Salaam kwa njia ya barabara, afanye
hivyo ili mle anamopita apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo
zifanywazo na wananchi. Sokoine hakufika Dar Es Salaam, mauti
yakamchukua kwa ajali ya gari pale Wami- Dakawa, Morogoro.

Leo
tuna viongozi wa wananchi wenye kutanguliza mbele maslahi yao binafsi.
Viongozi wasiotosheka na posho ya elfu sabini ya kikao. Viongozi wenye
kufikiria tu ’ kamuhogo kao’. Wanafikiri magari na marupurupu yao badala
ya masuala yenye kuwahusu  wananchi wa kawaida.



Je, Sokoine angefufuka leo ingekuwaje?
Bila
shaka angefufuka na kufa tena ndani ya siku saba. Maana, Sokoine
angeshangaa kuwaona wabunge wa leo wakichukua posho  ya kikao cha siku
moja sawa na mshahara wa miezi miwili au mitatu kwa Watanzania walio
wengi.
 



Sokoine angeshangaa kuona
wabunge hawatembelei tena Landrover za bei nafuu bali magari ya kifahari
huku wananchi walio wengi bado wanaishi kwenye nyumba za udongo na
nyasi. Kwamba bado kuna wanyonge wengi wasio na hakika ya kula yao ya
leo na kesho huku wananchi wakiambiwa, tena na Spika wa Bunge, kuwa
Bunge ni eneo la umasikini!



 Sokoine angeshangaa
kusikia kuwa uongozi siku hizi unanunuliwa, na hata yeye akijaribu tena
kuingia Bungeni atalazimika agawe ’ Vimuhogo’ kwa watakaompitisha kwenye
kura za maoni.  Sokoine angeshangazwa pia kusikia, kuwa kuna mawaziri
na watendaji wakuu serikalini wanaokaa mahotelini kwa kukosa nyumba za
serikali kwa vile umepitishwa uamuzi wa kuziuza, kisha kujenga nyingine
na kuziuza tena! 



Lakini, Sokoine angeshangaa
zaidi kuona Watanzania aliowaacha mwaka 1984 wamechelewa sana kuamka na
kupambana kuibadili hali iliyopo. 



Naam, Sokoine angefufuka
leo, angesononeka sana kuona pengo pana  lililopo kati ya wenye nacho na
wasio nacho. Kati ya viongozi na wananchi. 



Edward Moringe Sokoine, Daima Tutakukumbuka.
Mjengwa Maggid

No comments: