Friday, April 6, 2012

MAGGID MJENGWA NA TAFSIRI YAKE KUHUSIANA NA HUKUMU YA GODBLESS LEMA.


Ndugu zangu,
Kuna kila dalili, kuwa tunakokwenda ni kubaya. Tumefika mahala sasa, kuwa kwenye siasa tunaingiza hulka za ushabiki wa Simba na Yanga. Hii ni hatari kwa taifa.
Jana alhamisi, kabla ya jua la saa sita mchana, habari zililipuka na kusambaa kote nchini; Mahakama imemvua Ubunge Godbless Lema.
Ni ukweli, Godbless Lema ni mbunge kijana na maarufu sana hapa nchini. Lakini, imefika wakati Watanzania tukubali na tuamini, kuwa Mahakama inafanya kazi kama mhimili huru wa dola hata kama kunahitajika, kupitia Katiba mpya ijayo,  kuboresha mhimili huo ili uaminike zaidi.
Ni kwa mantiki hiyo, kuwa mahakama ni mhimili huru wa dola, tumeshuhudia  hata Serikali ikifikishwa Mahakamani na hata kushindwa kesi. Tumeshuhudia , katika historia ya nchi hii,  Wabunge wa CCM , bila kujali majina na umaarufu wao wakifikishwa mahakamani na kushindwa kesi.
Kwa Godbless Lema,  kutoa hadharani madai kuwa Rais wa nchi anahusika na hukumu yake ni kauli ya bahati mbaya sana anayopaswa yeye mwenyewe Lema, na chama chake, kuacha kuendelea kuitoa, hana maintiki. Inaidhalilisha Mahakama. Ni kauli iliyotolewa kwa haraka na isiyo na tija kwa taifa.
Tukubali kwa sasa, kuwa kule Arusha hukumu imeshatolewa. Kuna fursa pia ya kukata rufaa ya hukumu hiyo kwenye Mahakama iliyo juu zaidi. Hakika, kwa Godbless Lema na chama chake, huu ni wakati kutafakari hukumu hiyo na kuona ni namna gani ya kwenda mbele kisheria au kisiasa.
Haiwezekani kwa sasa kudai kuwa CCM inahusika na hukumu hiyo. Wakati kimsingi CCM imepata ’hasara nyingine ya kisiasa’  kwa matokeo ya  hukumu hiyo. Kwa anayechambua kwa undani sana, hukumu ya Lema ya kuvuliwa ubunge imekuja katika wakati mbaya sana kwa chama tawala, CCM.
Ni hukumu inayomtangaza na kumwongezea umaarufu Godbless Lema na chama chake cha Chadema.  Leo, bila kufuatilia mwenendo wa kesi husika,  kuna wanao-sympathy na Godbless Lema na Chadema, wakiamini CCM  imetumia Mahakama kumhujumu Godbless Lema na Chadema. Na kama Lema atasimama tena kuwania kiti hicho, basi, yumkini kura zake zitaongezeka maradufu. Lema ana hakika ya kura nyingi pia za ’ kuonewa huruma’.
Na ukweli mwingine ni huu, katika nchi yetu kwa sasa kuna kundi jipya la wapiga kura. Hawa naweza kuwaita ” Wapiga kura dhidi ya hali iliyopo”- Aina hii ya wapiga kura inaundwa kwa idadi kubwa na waliokuwa wapiga kura wa CCM katika chaguzi za miaka ya nyuma na ambao sasa hawaridhiki na hali iliyopo ndani na nje ya chama chao.
Ndio, hawa ndio waliokuwa wapiga kura wa CCM na ambao sasa  wanawachanganya sana CCM. Ndio hawa waliompigia kura Nassari Arumeru, ndio hawa waliowahakikishia viti vya udiwani Chadema kule Ruvuma, Mwanza na Mbeya.
Maana, ni wapiga kura wa kundi hili unaoweza kuwaona  wakijaa kwenye mikutano ya kampeni za CCM, lakini, kwa vile hawapati majibu ya maswali yao ya namna gani CCM na Serikali yake, si tu itakavyorekebisha, bali inavyorekebisha sasa ’ Hali iliyopo’, basi, siku ya kupiga kura wanatumbukiza kura zao kwa wapinzani.
Ndio, ni ukweli pia , kuwa ’ Ndani ya nyumba ya CCM’ kwa sasa  hakuna  amani na utulivu. Makundi na mbio za kuelekea kwenye  Urais 2015 zinawaacha wana-CCM wakivurugana wenyewe kwa wenyewe.
Focus sasa haiko kwenye kutekeleza ahadi lukuki walizowaahidi wapiga kura kwenye kampeni zilizopita. Kwa sasa kuna wenye kufikiria hatma zao za uongozi. Kuna waliojikita kwenye mnyukano wa kimakundi kwenye vita ya kuelekea Urais wa 2015.  CCM ya sasa inaonekana kuwa mbali na wananchi na kero zao zinazowakabili.  CCM ya sasa imeacha kuwa ‘ Kimbilio la Wanyonge’ kama wakati mmoja alivyopata kukiri Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. CCM ya sasa ni kimbilio la ‘ wenye nacho’ wakiwamo wafanyabiashara.
Ndio, CCM imeanza kulipa gharama ya wananchi kutoridhika na ’ Hali iliyopo’.

2 comments:

Anonymous said...

Huo ni mtazamo wako finyu tu, Kumbuka katibu mkuu wa ccm Mh.Mkama alisema makundi sio sababu ya kushindwa kwao mbona sasa wewe ukazana katika hilo.
Pia sihamini kuwa hao wazee wa zamani ndo wamekipigia kura chadema la asha.!! kuna kundi la vijana limejitokeza sasa linye upeo wa ajabu sana na wenye uwezo wa kulinganisha ukweli na uongo ndo sababu ya chadema kushinda kama wewe undhani wasaliti wa ccm ndo wamekipa ushindi chadema basi na wewe ni mmoja wapo. Dunia kwa sasa imebadilika watu na mitazamo mipya....katika historia ya hapa Duniani hakuna tawala na mfalume aliye kalia madaraka milele.. keep it.
Hata ccm mda wao ni sasa wa kupumzika na sio makundi. Kumbuka msemo huu ''siku ya mwizi ni harobaini'' na msemo huu '' siku ya kifo cha nyani miti yote uteleza''
Majid fikiria upya.

Anonymous said...

Mjengwa acha kuandika cheap news. Kila mtu anajua kauli ya Lema ni kutaka kuishughulisha ikulu na sio kuwa inamashiko ya aina yoyote. Sasa sijaona hoja yoyote ya maana uliyotoa zaidi ya kuongea vitu ambavyo hata mtoto wa la pili anavijua. Fikiri kwa makini achana na kuandika cheap news. hizo waachie waandishi wa habari chipukizi labda.