Saturday, April 14, 2012

TAMWA yapeleka waandishi habari za uchunguzi vijijini



Waandishi wa habari za uchunguzi juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia (GBV) kutoka vyombo mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja katika ofisi za TAMWA jijini Dar es Salaam kabla ya safari ya kuelekea mikoa mbalimbali kufanya kazi hiyo.

Na Joachim Mushi- Dar es Salaam

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimeteua baadhi ya waandishi wa habari za uchunguzi masuala ya ukatili wa kijinsia (GBV) kwa lengo la kuwapeleka katika mikoa 20 ya Tanzania Bara na Visiwani kuandika habari za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Akizungumza mapema jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wanahabari hao, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya amesema jumla ya wanahabari 18 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wanakwenda kufanya kazi hiyo, ambapo wamepangiwa wilaya moja kwa kila mkoa.

Amesema wanahabari hao pamoja na mambo mengine wanakwenda kufanya uchunguzi juu ya habari za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto vitendo ambavyo vimekuwa vikishamiri katika maeneo kadhaa ya nchi, huku vikikandamiza haki anuai za msingi dhidi ya jamii hiyo.

Bi. Nkya alisema uchunguzi huo utafanyika ndani ya siku 14 katika vijiji kadhaa, huku wanahabari wakifuatilia kwa kina vitende vya ubakaji, ukeketaji, vipigo kwa wanawake, utelekezaji familia pamoja na wanafunzi kukatishwa masomo na kuozeshwa.

Ameitaja mikoa ambayo waandishi wamepelekwa na wilaya zake kwenye mabano ni pamoja na Morogoro (Mvomero), Mtwara (Newala), Shinyanga (Kahama), Dar es Salaam (Ilala, Temeke na Kinondoni), Kilimanjaro (Same), Pwani (Mkuranga), Mara (Tarime), Manyara (Simanjiro), Tanga (Handeni), Kigoma (Kasulu), Iringa (Kilolo), Mbeya (Rungwe), Singida (Iramba), Dodoma (Kondoa), Arusha (Karatu), na Njombe (Njombe).

Kwa upande wa Zanzibar mikoa ambayo waandishi watafanya kazi hiyo ni pamoja na Kaskazini Pemba (micheweni na Wete), Kusini Pemba (Chakechake), Kaskazini Unguja (Kaskazini A na B, Kusini Unguja (Kusini Unguja) na Mjini Magharibi (Wilaya ya Kati).

No comments: