Monday, April 2, 2012

Makada 42 wa CCM kuchuana Ubunge EALA Dodoma kesho


MAKADA na wanachama 42 wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) kesho watachuana vikali kuwania nafasi 24 na baadae kuwania nafasi  8 kati ya 9 za kuiwakilisha Tanzania katika  Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wagombea hao watapigiwa kura na wabunge wa CCM Mjini Dodoma Aprili 3, mwaka huu na kubaki 24.

Mrisho Gambo, Adam Kimbisa, Makongoro Nyerere,  Dk Aman Kabourou , John Ngongolo, Dk Evans Rweikiza, Siraju  Kaboyonga, Bernard Murunya, Dk Edmond Mndolwa, Christopher Awinia na Dk Hilderbrand Shayo.

Wengine ni Handley Mafwega, William Malecela, Mussa Mnyeti, Elibariki Kingu, Simon Berege na Godfrey Mosha.

Waliopitishwa kwa upande wa wanawake kwa Tanzania Bara ni Shy-Rose Bhanji, , Fancy Nkuhi, Janeth Mmari, Janet Mbene, Norah Mukami, Shally Raymond, Ngollo Malenya, Godbertha Kinyondo, Hamidah Kalua, Angela Kizigha, Happyness Lugiko na Ruth Msafiri.

Wanaowania nafasi hizo kutoka Zanzibar, wanaume ni Dk Said Bilal, Abdallah Mwinyi, Dk Haji Haji, Dk Ahmada Khatib, Zubeir Maulid, Khamis Makame, Abdul Aziz Salim na Mbwana Mwinyi.

Aidha Wanawake ni Septuu Nassor, Safia Rijaal, Rukia Msellem, Sabah Ali na Maryam Yahaya.

Nape, alisema kura hizo za wabunge wa CCM zitasimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Dogo Mabruki pamoja na yeye mwenyewe Nape Nauye.

Wabunge waliokuwa kwenye Bunge linalomaliza  muda wake ni Dk George Nangale, Abdullah Mwinyi, Kate Kamba, Dk  Kabourou, Fortunatus Masha, Dk Didas Massaburi, Bilal na Sebtuu Nassor.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila alisema hivi karibuni kwamba uchaguzi wa wajumbe tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge hilo la EALA utafanywa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia Aprili 10 hadi 20, mwaka huu. 

Alisema uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia kuwa muda wa Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006, utafikia ukomo wake Juni 4, 2012.

Kwa mujibu wa kanuni, Katibu wa Bunge ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo na atapaswa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni Aprili 10 na siku ya uchaguzi, Aprili  17.

Katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea wa vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni kuhusiana na uchaguzi huo kwa ajili ya kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata wagombea kupitia vyama hivyo ambao majina yao yatawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.
Habari kwa Hisani ya Father kidevu Blog

No comments: