Sunday, April 15, 2012

Mawaziri, wabunge waongoza kusamehewa kodi



CAG Ludovick Utouh
Na Daniel Mjema,Dodoma
SIKU chache baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti yake bungeni ikionyesha ongezeko la misamaha ya kodi, imebainika kuwa mawaziri na wabunge ni miongoni mwa vigogo wanajinufaisha na Sheria ya Msamaha wa Kodi kinyume cha taratibu.

Orodho ya majina ya watu waliosamahewa kodi na Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 iliyopo katika tovuti ya Wizara ya Fedha, inaonyesha majina ya baadhi ya mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali wakiwa wamenufaika na misamaha hiyo.

CAG Ludovick Utouh katika ripoti yake, anasema misamaha ya kodi iliyotolewa kwa taasisi mbalimbali, hadi kufikia Juni 30,2011 ni Sh1.02 Trilioni na kueleza kuwa eneo hilo la misamaha ya kodi linapaswa kutazamwa ili kuepuka kuwa na makusanyo pungufu ya kodi.

Hatua ya Serikali kuruhusu kutolewa kwa misamaha ya kodi inayofikia asilimia 18 ya makusanyo yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewashtua wananchi, wasomi na wanasiasa ambao sasa wanahoji umakini wa Serikali.

Katibu Mkuu

Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhan Kijjah aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa misamaha ya kodi ipo kisheria na kwamba kila mmoja ana haki ya kuipata.

"Misamaha ipo kisheria, watu wote wanapata kulingana na sheria iliyopo, hakuna upendeleo," alisema Katibu Mkuu huyo.

Alisema katika mwaka wa fedha ujao, watapitia upya Sheria ya Misamaha ya Kodi kuona kama ina upungufu ili ifanyiwe marekebisho kwa lengo la kuongeza mapato ya kodi.

Kijjah alisema kamati ya kuangalia mapato, itapitia upya sheria hiyo kubaini udhaifu wake na itapendekleza nini cha kufanya.

Kuhusu tuhuma zilizotolewa na CAG katika ripoti yake bungeni, alisema hawajapata ripoti yake na kwamba wanaisubiri ili waipitie na kumpatia majibu.

Alisema wanatarajia kupata ripoti hiyo wiki ijayo na kuifanyia kazi kwa mwezi mmoja kabla ya kumkabidhi.


Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG,) inaonyesha kuwa kiwango hicho cha misamaha ya kodi kilichotolewa mwaka 2010/2011 ni cha juu ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Alifafanua kuwa taarifa za TRA zilionyesha kuwa misamaha ilitolewa kwa taasisi mbalimbali yenye thamani ya sh1,016,320,300,00 ambazo ni sawa na asilimia 18 ya makusanyo yote nchini.

Kwa mujibu wa Utouh, kama kiasi hicho kisingesamehewa, TRA ingekusanya Sh6.5 trilioni  sawa na Sh717.4 bilioni zaidi ya kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ambacho ni Sh6,566,525,544,378.

“Siku zote tumekuwa tukipiga kelele kuhusu misamaha ya kodi ingawa tunasema misamaha ya kodi haiepukiki lakini lazima isimamiwe na iwe ni lazima kutolewa…kwa kweli eneo la misamaha ya kodi ni la kutazamwa,”alisema.

Utouh alisema misamaha hiyo ya kodi ya asilimia 18 ni ya juu sana ukilinganisha na viwango vya misamaha ya kodi vinavyotolewa nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda na kutaka suala hilo litazamwe kwa macho mawili.

Orodha ya watu walionufaika na misamaha ya kodi kuanzia mwaka 2006 hadi 2008 iliyopo katika tovuti ya Wizara ya Fedha inajumuisha baadhi ya mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa idara za Serikali na baadhi ya wafanyakazi wa Ikulu.

Hoja hiyo ya misamaha ya kodi imeibua mijadala mbalimbali nchini huku Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema) akihoji sababu ya kutolewa kwa kiwango hicho kikubwa cha msamaha na kutaka waliosamehewa watajwe.

“Watajitetea kuwa wametoa misamaha ili kuvutia wawekezaji lakini tujiulize hivi kwani hizo nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zenyewe hazivutii wawekezaji?... Hizo fedha zingepelekwa kwenye miradi ya barabara tungekuwa wapi? Alihoji.

Mbunge huyo alimtaka Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo kuwataja watu au taasisi zilizonufaika na misamaha hiyo ili Watanzania watumie orodha hiyo kupima kama watu na taasisi hizo, zilistahili kupata misamaha hiyo ya kodi.

Mbunge mmoja wa CCM ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alidai kinachoonekana ni kuwa Waziri Mkulo hana uzalendo na nchi kwa sababu haiwezekani atoe misamaha ya kodi na hapo hapo deni la taifa liendelee kukua.

“Taarifa ya CAG inaonyesha deni la taifa limekua hadi kufikia Sh14.4 trilioni sasa tunajiuliza hivi inaingia akilini kweli? Tunashindwa kujitegemea katika bajeti hapo hapo tunatoa misamaha ya ajabu, hivi hii nchi kweli itakwenda?”Alihoji.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma wiki hii, Utouh alisema deni la taifa limeongezeka kutoka sh10.5 trilioni mwaka wa fedha wa 2009/2010 hadi kufikia sh14.4 trilioni mwaka 2010/2011 sawa na ongezeko la asilimia 38.

“Kuna ongezeko kubwa la deni la taifa lakini hoja hapa si kuongezeka kwa deni la taifa bali ni kwamba deni hili limeletwa kwa mikopo yenye manufaa kwa taifa na yenye kukuza uchumi wa nchi? Hii ndio hoja ya msingi ya kuangalia,” alisema.

Mara baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu(PAC), John Cheyo alionyesha kushangazwa na kuendelea kukua kwa deni la Taifa wakati miradi mingi nchini haina fedha.

“Deni la taifa linatupa matatizo sisi wote hapa kwa sababu mimi sielewi maana tunakopa lakini miradi yetu haina pesa hapa kuna kitendawili,”alisema Cheyo na kusema Bunge itabidi lijadili na kutegua kitendawili hicho.

Mwananchi

No comments: