Sunday, April 15, 2012

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF) LEO


MGAMBO SHOOTING YAPUNGUZWA KASI FDL

Fainali ya 9- Bora ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao imeendelea kushika kasi leo (Aprili 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro kwa Mgambo Shooting ya Tanga kuvutwa shati.

Mgambo Shooting ambayo hadi kabla ya mechi za leo (Aprili 15 mwaka huu) ilikuwa ikiongoza kwa pointi 11 imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na Polisi Tabora ambayo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika ilikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Mabao ya Polisi Tabora yalifungwa dakika ya tano na Ernest Nkandi kwa shuti kali lililomshinda kipa Kulwa Manzi. Keneth Masumbuko aliifungia Polisi Tabora bao la pili dakika ya 40.

Mgambo Shooting inayofundishwa na beki wa zamani wa Taifa Stars, Joseph Lazaro ilikianza kipindi cha pili kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao dakika ya 58 lililofungwa kwa shuti kali nje ya eneo la hatari na Salum Kipaga.

Dakika saba kabla ya filimbi ya mwisho, Juma Mwinyimvua aliipatia Mgambo Shooting bao la kusawazisha akimalizia pasi ya Fully Maganga kutoka wingi ya kushoto.

Fainali hiyo inashirikisha timu tisa ambapo tatu za kwanza zitafuzu kucheza VPL msimu ujao. Timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ni Rhino Rangers ya Tabora, Trans Camp ya Dar es Salaam, Mbeya City, Tanzania Prisons ya Mbeya na Mlale JKT ya Ruvuma.

No comments: