Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Nape Nnauye 
---
Hivi  karibuni chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilielezea kile  ilichoeleza kuwa ni kutishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya  nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya  Igunga peke yake.
Madai  hayo ya CHADEMA, pamoja na wanachama wengine na mashabiki wao,  yalitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, ambaye alidai  kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo kwa madai yao  imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka  kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua  kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam Aprili 29  mwaku huu mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu wanne  kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru mkoani  Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke  yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mwaka jana.
Mbowe  katika maelezo yake alijaribu katika maeneo kadhaa kuihusisha CCM na au  serikali yake katika matukio kadhaa yaliyowakabili baadhi ya wanachama  na viongozi wa Chadema katika maeneo mbalimbali nchini likiwemo lile la  Mbunge Highness Kiwia ambaye Suala lake bado Lipo mikononi mwa vyombo  Vya dola likishughulikiwa.
Katika  sehemu kubwa ya maelezo ya Ndg. Mbowe amejitahidi kuonesha kuwa mauaji  yote yaliyoikabili na yatakayokuwa yakiikabili Chadema kupitia wafuasi  wake yanafanyika kisiasa, Jambo ambalo ni la uzushi, kwani Halina  ushahidi wa kisheria hata kimazingira, wa Moja kwa Moja unaoondosha  ujinai au makosa hayo, na kuwa ni makosa yanayolenga muktadha wa  kisiasa.
Huku  akitaka kuuaminisha umma kuwa huo ndio ukweli, Ndg. Mbowe amesisitiza  kuwa hilo lime kuwa likitekelezwa na CCM kwa lengo la kuwatisha wananchi  kujiunga na chama hicho hoja ambayo haina msingi wowote wa kiutafiti.
Hivyo  CCM kwa kutambua kuwa Suala la mauaji linabeba Kosa la jinai, na kwa  kuwa Ndg. Mbowe ameshutumu Moja kwa Moja CCM na serikali yake kuihusisha  na mauaji hayo, ni vema sasa nasi tukatoa msimamo wetu dhidi ya tuhuma,  hiyo.
Kwanza,  si busara hata kidogo kuihusisha CCM katika matukio hayo, kwani  uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola umeshindwa mpaka sasa kuhusisha  matukio hayo na siasa, badala ya kuyahusisha na makosa ya jinai ambayo  hufanywa na watu kwa malengo tofauti na yale ambayo Ndg. Mbowe anataka  kuwaaminisha watu.
Pili,  CCM haijawai, haiwezi, na haitakuja fanya jambo lolote lenye lengo la  kuvuruga Amani na Usalama wenye utulivu ndani ya taifa letu, hivyo  uzushi na usingiziaji uliofanywa na Mtu Kama Ndg. Mbowe, si vema kuuacha  kimya, badala yake nimetumia wasaa Huu muhimu Kujibu, na kutoa  ufafanuzi ili Kuupa umma wa watanzania habari sahihi.
Ni  aibu kwa Chama kama Chadema kujitahidi kwa nguvu zote kujaribu kuficha  ukweli wa mauaji yanayotoa roho za watanzania wenzetu kwa kuyapa sura ya  kisiasa. Hizi ni juhudi za makusudi za kutaka kuficha ukweli wa  kinachotokea.
Ni  aibu kwa chama kama Chadema kujaribu kutumia mauaji mabaya kama haya  kutafuta mtaji wa kisiasa. Huku ni kuonyesha jinsi gani wamefilisika  kisiasa mpaka wanafikia mahali pa kuamini kuwa wanaweza kutumia chochote  kama mtaji wa kisiasa, vikiwemo vifo vya watanzania wenzetu. Huku si  kufilisika tu ila kwakweli ni unyama unaotakiwa kulaaniwa na kila  muungwana.
Mwisho.
Imetolewa na:
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM
No comments:
Post a Comment