
Timu  ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) itacheza na Zimbabwe katika mchezo  wa kirafiki utakaofanyika Mei 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar  es Salaam.
Twiga  Stars hivi iko katika ziara ya mechi za kirafiki katika mikoa ya Dodoma  na Mwanza. Leo (Mei 8 mwaka huu) itacheza na kombaini ya Mkoa wa Dodoma  ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 katika mchezo utakaofanyika  Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.
Kesho  (Mei 9 mwaka huu) itaondoka kwenda jijini Mwanza ambapo pia itacheza  mechi moja ya kirafiki Mei 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, na  kurejea Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe.
Zimbabwe  inatarajia kuwasili kesho (Mei 9 mwaka huu) jioni kwa ndege ya South  African Airways (SAA) ikiwa na msafara wa 25 na wataondoka Mei 14 mwaka  huu alfajiri. 
KAMATI YA MASHINDANO KUPANGA VITUO LIGI YA TAIFA
Kamati  ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia  kukutana leo (Mei 8 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine itapanga  vituo vya Ligi ya Taifa na tarehe ya kuanza ligi hiyo.
Mikoa  nane imeomba kuwa wenyeji wa ligi hiyo itakayochezwa katika vituo  vitatu. Mikoa hiyo kupitia kwenye vyama vyao vya mpira wa miguu ni  
Mikoa iliyoomba vituo ni Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mbeya, Shinyanga na Singida.
Timu  zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa wa mikoa. Timu hizo ni Ashanti  United ya Ilala (Dar es Salaam), Aston Villa (Singida), Bandari FC  (Kagera), CDA (Dodoma), Flamingo SC (Arusha), Forest FC ya Siha  (Kilimanjaro), JKT Kanembwa (Kigoma), Korogwe United ya Korogwe (Tanga),  Kurugenzi ya Mafinga (Iringa), Lindi SC (Lindi) na Majimaji (Tabora).
Mighty  Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers ya Kilombero (Morogoro), Mpanda Stars  ya Mpanda (Rukwa), Mwadui FC (Shinyanga), Nangwa VTC (Manyara), Ndanda  FC (Mtwara), Pamba SC (Mwanza), Polisi Mara (Mara), Red Coast ya  Kinondoni (Dar es Salaam), Super Star ya Bagamoyo (Pwani), Tenende SC  (Mbeya) na Tessema FC ya Temeke (Dar es Salaam).
KILA LA KHERI SIMBA, PONGEZI
Shirikisho  la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Simba  kwenye mechi yake ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly  Shandy ya Sudan itakayochezwa Jumapili (Mei 13 mwaka huu).
Mechi  hiyo itachezwa katika mji wa Shandy kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa  za Afrika Mashariki. Simba inaondoka kesho kwenda huko kwa ndege ya  Kenya Airways.
Msafara  wa timu hiyo utaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Hussein  Mwamba, na unatarajia kurejea nyumbani Mei 15 mwaka huu.
Pia  TFF inaipongeza Simba kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya  Vodacom (VPL) ambayo Mei 6 mwaka huu ilifunga msimu wa 2011/2012.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment