Friday, May 25, 2012

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII:SHERIA HAIRUHUSU VIBALI KUUZWA KWENYE SHAMBA LA SAO HILL

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
 WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
--
 SHERIA HAIRUHUSU VIBALI KUUZWA KWENYE SHAMBA LA SAO HILL
Wizara ya Maliasili na Utalii inafafanua kuwa uvunaji wa Miti katika Shamba la Sao Hill unafuata utaratibu uliowekwa kisheria.
Sheria ya Misitu haimzuii mwananchi yeyote kuvuna mazao ya misitu kutoka kwenye misitu ya asili au ya kupandwa mradi awe amefuata sheria na taratibu zilizopo katika nyaraka husika, na hakuna nyaraka yoyote inayoagiza kwamba vibali vya uvunaji vigawiwe kwa viongozi ama watumishi wa serikali ili waviuze.


Ufafanuzi huu unatolewa kufuatia habari zilizoandikwa na gazeti moja kuwa vigogo wa Maliasili ndiyo wanaochukua vibali na kuviuza kwa wateja. Habari hiyo haina msingi maana utaratibu unaotumika unatekelezwa kwa uwazi na unajulikana kwa wateja wa mazao ya misitu.
Shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu hufanywa kwa kufuata ‘Mwongozo wa Uvunaji Endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu’ wa mwaka 2007, ambao unaonyesha taratibu muhimu za kufuatwa katika shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu.


Mwongozo huo unatokana na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, pamoja na Matangazo ya Serikali (Government Notices) Namba 69 na 70 ya mwaka 2006.


Shughuli za ugawaji wa mazao ya kuvuna katika kila shamba la Serikali hufanywa na Kamati ya Ugawaji Mazao ya Misitu ya sehemu husika.


Utaratibu uliopo ni kuwa mwananchi anayehitaji mazao kutoka katika misitu ya mbao laini, kama ile ya Sao Hill, hupeleka maombi yake kwa Meneja wa shamba linalohusika, kuanzia Januari 1 hadi tarehe 30 Aprili kila mwaka. Maombi hayo yanatakiwa yapokelewe mapema maana Kamati ya Ugawaji hufanya kikao chake mwezi Juni kila mwaka.
Aidha mwongozo wa uvunaji unaotumika hivi sasa unatanabaisha kuwa kipaumbele kitatolewa kwa mwombaji mwenye kiwanda lakini sio lazima awe na kiwanda.


Hata hivyo, taratibu hizo za uvunaji zimefanyiwa marekebisho yatakayoanza kutumika mwaka ujao wa fedha ambapo mwombaji sasa atalazimika kuwa na kiwanda ili aweze kupata kibali. Utaratibu huu ulitangazwa kwenye vyombo vya habari na tovuti ya Wizara www.mnrt.go.tz.


Katika utaratibu huo mpya Wizara itandaa utaratibu maalumu wa kuhakikisha wanavijiji wanaopakana na misitu ya serikali inayovunwa wananufaika na misitu hiyo kwa kuwa wanachangia kuilinda.


George Matiko
MSEMAJI WA WIZARA
Tarehe 24 Mei 2012
Simu - 0784 468047

No comments: