Tuesday, October 11, 2011

BILA YA UWEZESHAJI WA MWANAMKE WA KIJIJINI USAWA KWA WOTE NI NDOTO-MH. SOPHIA SIMBA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba (Mb) akizungumza kwa niaba ya Nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakati wa mkutano wa siku tatu wa Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya wanawake. Akizungumza kwa niaba ya nchi hizo, Waziri Simba pamoja na mambo mengine ametilia mkazo uwezeshwaji wa wanawake wa vijijini kama njia sahihi ya kuwapatia fursa sawa wanawake wote katika nchi za SADC.

Na Mwandishi Maalum

New York

Uwezeshwaji wa mwanamke hususani katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika ( SADC) hauwezi kuwa kamili kama mwanamke wa kijijini hatawezeshwa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye dhamana ya Maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, Mhe. Sophia Simba(MB),wakati alipokuwa akizungumza kwa niaba ya nchi za SADC katika mkutano unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa ukijadili hali ya wanawake zikiwamo fursa za maendeleo

Mhe. Waziri Sophia Simba (MB)anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa siku tatu utakaojadili na kubadilishana mawazo, kupeana mbinu na mikakati katika masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya wanawake.

Aidha washiriki wa mkutano huo wakiwamo mawaziri kutoka nchi mbalimbali pia watapokea na kujadili taarifa kuhusu uondoshaji wa ubaguzi dhidi ya wanawake,uboreshaji wa hali ya wanawake wa vijijini, unyanyasaji dhidi ya wanawake wafanyakazi wahamiaji na ukatili dhidi ya wanawake.

Mkutano huo unafanyika chini ya Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa. Kamati hiyo inahusika na, pamoja na mambo mengine, ustawi na haki za binadamu, utamaduni, misaada ya kibinadamu, fursa na haki za wanawake, watoto na makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo wazee na watu wasiojiweza.

Waziri Simba amewaeleza wajumbe wanaohudhuria mkutano huo kwamba, uwezeshaji wa mwanamke wa kijijini ni suala muhimu katika nchi za SADC hasa ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya wanawake katika nchi hizo wanaishi vijijini huku wakikabiliwa na umaskini uliokithiri.

“Hatuwezi kufikia malengo kamili ya uwezeshwaji wa wanawake kama hatutawawezesha wanawake wa vijijiji, na hasa ikizingatiwa kwamba bado walio wengi hawana fursa za kumiliki raslimali ikiwamo ardhi, mifugo, mitaji na teknolijia za kisasa” akasema Mhe. Waziri

Na kuongeza.“Ndiyo maana sisi katika SADC tunaamini kwamba uwezeshaji wa mwanamke hauwezi kufanikiwa bila ya kushughulikia changamoto za uboreshaji wa hali ya wanawake wa vijijini”.

Aidha, Waziri Simba amebainisha kwamba ingawa nchi hizo za SADC zimepata mafanikio makubwa, katika kuleta usawa wa kijinsia kupunguza ubaguzi na unyanyasaji kwa kutelekeza mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.Bado nchi hizo zinakabiliwa na kuwapo kwa pengo kubwa kati ya utekelezaji na uwajibikaji.

Akasema kuwa hali hiyo, pia inachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwapo kwa mkanganyiko baina ya sheria za kimila, sheria za kitaifa na zile za kimataifa.

Kama hiyo haitoshi, Waziri anaongeza kuwa hata uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya juu vya utoaji maamuzi bado ni mdogo katika baadhi ya nchi za SADC.

“Bado uwakilishi wa wanawake ni mdogo katika baadhi ya nchi zetu. Ujinga na umaskini kwa wanawake na watoto wa kike bado ni kikwazo kikubwa katika kufikia usawa wa kijinsia. Tunahitaji juhudi za makusudi katika kukabiliana na changamoto hizi” amesisitiza.

Wakati huo huo, Waziri Sophia Simba amesema kuwa nchi za SADC zinatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na wanawake wa vijijini kupitia kilimo.

Ameeleza kuwa nchi hizo zinatiwa moyo na namna Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linavyoendelea kutoa kipaumbele katika uboreshaji wa hali ya wanawake wa vijijini.

Akatumia nafasi hiyo kukaribisha taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inayoelezea kwamba kumekuwa na hali ya kuridhisha katika maendeleo ya wanawake wa vijijini katika ujumla wake.

“ Kwa niaba ya nchi za SADC napenda pia kutumia fursa hii kulishukuru Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa ( FAO) kwa mchango wake wa kuwapatia wanawake mafunzo ya kilimo katika nchi za Msumbiji, Swaziland, Zambia na Tanzania”

Aidha akasema nchi za SADC pia zimefarijika na uamuzi wa Kamisheni kuhusu hali ya wanawake ya kutoa kiupaumbele suala la uwezeshaji wa wanawake katika ajenda yake ya mwaka 2012.

Akasema kuwa uamuzi wa kamisheni hiyo utatoa fursa ya kutathimini mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa malengo na mipango mbalimbali inayolenga kumwezesha mwanamke. Vilevile kubaini mbinu za kuchagiza utekelezaji wake.

No comments: