Thursday, March 15, 2012

Mkono aapa kufia ubunge



Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM),
Nimrod Mkono
 


Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, amesema kuwa hana nia ya kustaafu ubunge na kwamba kifo ndicho kitakamtoa katika nafasi hiyo.
Mkono alisema hadi sasa hajaona mtu wa kumwachia jimbo hilo ambaye anaweza kutimiza ndoto zake za kuifanya Butiama kuwa wilaya mpya na kuwa maarufu kama Washington DC, Marekani.
Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijiji kwa vipindi vitatu sasa, alitangaza hatua hiyo katika Kijiji cha Mwibagi, Kata ya Kianyari jimboni humo  wakati akihutubia wananchi wa kabla ya kukabidhi jengo la ofisi ya kijiji na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alilolikarabati kwa zaidi ya Sh. milioni 10.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakijitokeza kugombea ubunge kwa kutanguliza mbele maslahi yao badala ya kutumia uwezo wao kuharakisha maendeleo ya wananchi huku wakiendelea kupiga kelele zisizo na tija kwa wananchi.
“Mimi si mbunge wa kupiga kelele kama hao mavuvuzela mnaowasikia, mimi nilikuja kugombea si kwa ajili ya tumbo langu bali nimetafuta nafasi hii ili kutumia uwezo wangu kushirikiana nanyi kuharakisha maendeleo yetu,” alisema na kuongeza:
 “Hivyo siwezi leo kuacha ubunge kwa kumuachia mtu ambaye hawezi kutimiza ndoto zangu za kufanya eneo lote la wilaya yetu mpya ya Butiama kuwa Washington DC na kuwa kielelezo tosha cha kuonyesha sehemu aliyozaliwa Baba wa Taifa letu,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema yuko tayari kufananishwa na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kung’ang’ania madarakani, lakini lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa jimbo la Musoma Vijijini na Butiama kuwa kielelezo tosha cha maendeleo ndani na nje ya nchi.
Mkono alisema anashangazwa na watu wanaoutaka ubunge kwa ajili ya kuganga njaa zao bila kujali kwanza wananchi waliowawezesha kufika hapo na wengine baada tu ya kupata nafasi hizo wamekuwa wakikaa mijini kwa lengo la kuwakwepa wapiga kura wao, jambo ambalo limewachukiza wananchi na kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya wabunge kila baada ya miaka mitano.
Aliwashauri wenye ndoto za kugombea ubunge katika jimbo hilo kabla ya kufanya hivyo waanze kufanya ziara za kitalii katikaili kujionea yaliyotekelezwa katika uongozi wake.
“Nilikuja mwaka 2010 katika kura za maoni na kundi la watu wakijiita ni wagombea ubunge eti wana nia ya kuleta maendeleo na niliwaambia hawa watu ni watalii na leo mmewaona wako wapi?” alihoji na kuongeza:
“Kazi hii ya ubunge inahitaji moyo wa dhati kwa kuumwa na umasikini wa wananchi unaowaongoza si kufikiria ukipata nafasi hiyo utajazaje tumbo lako?”
Mkono alisema wabunge wengi waliingia katika nafasi hiyo bila kutafakari kwa kina ili kujua shida zinazowakabili wapiga kura wao, kitu ambacho kwa sasa kimeanza kuwapa shida na kufikia hatua ya kutaka kuyakimbia majimbo yao.
Aliwaambia wananchi hao kuwa ingawa amekuwa akitumia sehemu ya mapato yake kwa ajili kuharakisha maendeleo ya jimbo, lakini kamwe wasitegemee kila kitu watafanyiwa na wanasiasa wala serikali, bali kinachotakiwa ni kukaa na viongozi wao wakiwemo madiwani kwa ajili ya kuzitambua changamoto zinazokabili maeneo yao na kuweka mipango inayoweza kutekelezeka kwa wakati.
Alisema kitu ambacho amekuwa akikilisisitiza katika kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo ni kuwezesha kila mzazi kusomesha mtoto wake, jambo ambalo lilimgusa na kuamua kujenga shule nyingi za sekondari na hivi sasa mkazo mkubwa ameuelekeza katika ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Butiama.
“Nimeshukuru sana serikali kutupatia Wilaya ya Butiama, hii itaniwezesha nami kukazania maendeleo ya wilaya hii. Kuna mengi yalisemwa kuhusu wilaya hii, lakini ni ukweli hatuwezi kuiacha Butiama ikapotea na ili isipotee, lazima serikali iwe karibu na eneo hilo na kwa kuanzia, nimejenga katika maeneo hayo shule nzuri kuliko shule zozote nchini na sasa nguvu naelekeza katika ujenzi wa nyumba za walimu katika shule zote za sekondari,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini, Magina Magesa, alimshukuru Mkono kwa kukarabati jengo hilo la ofisi za serikali ya kijiji na CCM ambalo liliezuliwa na upepo na kuongeza kuwa halmashauri inatambua mchango mkubwa wa kuharakisha maendeleo unaofanywa na mbunge huyo.
“Wakati Mkono anakuja kugombea ubunge, halmashauri yetu yenye kata 34 ilikuwa na shule tano tu za sekondari, leo tunazaidi ya 40 zikiwemo za kisasa za kidato cha tano na sita huku akiendelea na mipango ya kushirikiana na serikali kwa ajili ya kujenga Chuo Kikuu cha kumbukumbu ya Nyerere,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: